Sunday, April 18, 2010

 
PINDA AKAGUA UKARABATI WA RELI YA KATI


RELI ya Kati kutoka Dar es Salaam kwenda Kigoma na Mwanza iliyoharibiwa na mafuriko ya Desemba mwaka jana katika maeneo ya Kilosa na Mpwapwa inatarajiwa kuanza kazi tena katikati ya mwezi ujao, Waziri wa Miundombinu, Dk.Shukuru Kawambwa ametangaza leo (Jumapili Aprili 18, 2010).

Akitoa maelezo mbele ya Waziri Mkuu Mhe. Mizengo Pinda aliyekagua ukarabati wa reli hiyo eneo la Gulwe, kilomita 101 Mashariki mwa Dodoma, Dk. Kawambwa alisema sehemu kubwa ya ukarabati imekwishakamilika na matarajio ni reli kuanza kazi Mei 14 mwaka huu.

Mipango ilikuwa inaandaliwa ili usafiri wa treni za abiria kwa reli ya kati uanzie na kukamilika Dodoma ambako kati yake na Dar es Salaam yatumike mabasi, lakini Waziri Kawambwa alisema maandalizi hayo yanaweza kukutana na reli iliyokuwa tayari Mei.

Utaratibu wa mabasi hadi Dodoma baadaye treni uliwahi kutumika mwaka 1998 wakati ulipotokea uharibifu mkubwa kutokana na mafuriko, eneo la Kilosa.

Hivi sasa usafiri wa abiria kati ya Dar es Salaam na Kigoma na Mwanza ni kwa mabasi. Kwa kwenda Kigoma ni kuzunguka kupitia Kahama, mkoani Shinyanga. Kwa mizigo ni kwa malori.

Dk. Kawambwa alisema maeneo 32 ya reli hiyo yaliharibiwa baada ya mafuriko hayo ya Desemba 28 hadi 31, mwaka jana na mpaka sasa maeneo 20 yamekwishakamilika na mengine yaliyobaki yanamaliziwa, Dk Kawambwa alisema.

Baadaye Waziri Mkuu alisafiri kwa treni umbali wa kilomita 17 na kuvuka kwenye eneo lililokamilika. Katika eneo alilopita la Chibibo, reli ilikuwa imezolewa na mafuriko na kuacha gema la kina cha mita 15 na urefu wa mita 200.

Ujenzi huo ulifanywa na kikosi cha ufundi cha Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Kampuni ya Reli TRL, tangu Februari 5 mwaka huu kwa upande wa Mpwapwa na Februari 16 kwa upande wa Kilosa, ambako mvua ilikuwa inaendelea.

Fedha ilizoombwa kwa kazi hiyo ni zaisi ya Sh. Bilioni 15 na tayari zidi ya Sh. Bilioni 10 zimekwishatolewa na kutumika.

Siku chache baada ya mafuriko hayo, Waziri Mkuu alikagua uharibifu uliofanywa katika eneo la Gulwe na kuahidi kuwa Serikali itagharimia urejeshaji wa huduma za reli na barabara zilizoharibiwa na mafuriko katika Wilaya ya Mpwapwa, mkoani Dodoma na Kilosa, mkoani Morogoro.

Waziri Mkuu alisifia kikosi cha JWTZ kilichohusika na ujenzi kwa kufanya kazi ya uhakika na kwa haraka kuweza kuirejesha katika hali ya kawaida reli ya kati ambayo ni muhimu kwa usafiri wa abiria na mizigo nchini.

Mhe. Pinda pia alikagua ujenzi wa daraja la barabara ya Gulwe ambao umekamilika na ujenzi wa daraja la Godegode la Barabara ya kilomita 60 inayounganisha makao makuu ya Wilaya ya Mpwapwa na Godegode na Lumuma.

Ujenzi wa daraja la Godegode litakalokuwa la makalavati makubwa katika eneo la mita 100 za kuvuka mto, unatarajiwa kuanza kesho (Jumatatu Aprili 19, 2010) na kuchukua miezi miwili kwa gaharama ya Sh. milioni 774.

Waziri Mkuu ambaye alikwenda Mpwapwa kwa gari asubuhi leo (Jumapili Aprili 18, 2010) alirejea Dodoma jioni ambako anahudhuria kikao cha Bunge.

Comments: Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?