Saturday, April 17, 2010
Waziri Mkuu, Mizengo Pinda akihutubia katika Tamasha la Kulipongeza Bunge na Serikali kwa kupitisha sheria ya kumlinda mtoto lililofanyika kwenye uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma, Aprili 17, 2010.
PINDA AHUTUBIA TAMASHA LA WATOTO LA KUUNGA MKONO BUNGE NA SERIKALI
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda amelaani vikali mauaji ya kiajabu ya watoto wadogo yaliyozuka hivi karibuni katika Tarafa ya Tukuyu Wilayani Rungwe mkoani Mbeya na kuahidi kuwa Serikali itachukua hatua kali kwa wahusika watakopatikana.
Alikuwa akihutubia baada ya kupokea maandamano ya watoto kupongeza Serikali na Bunge kwa kupitisha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009, kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Dodoma leo (Jumamosi Aprili 17, 2020).
Inasikitisha kuona kuwa watoto hao wadogo wanauawa ovyo kikatili katika namna ya kutisha huku watu wazima wapo na wanashindwa kuwalinda, alisema.
Mhe. Pinda alikumbusha kuwa matukio haya ya kuua watoto wadogo yanatokea baada ya wimbi la kuwaua walemavu wa ngozi, ambao nao wengi wao wanaowindwa ni watoto wadogo pia.
“Kila nikikaa sielewi. Watanzania tufike mahali kweli turejee na kusema matendo haya siyo ya kibinadamu, hayampendezi Mungu, hasa kuwaua watoto wadogo,” alisema.
Watoto wapatao sita wameuawa kikatili huko Tukuyu hivi karibuni na Polisi imewakamata watu kadhaa wakishukiwa kuhusika na mauaji hayo ambayo yanahusishwa na imani za kichawi.
Katika hotuba yake, Waziri Mkuu alisisitiza kuwa Serikali itahakikisha kwamba Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 itatekelezwa kudhibiti maovu mengi yanayotendwa dhidi ya watoto.
“Napenda kutoa tahadhari kwamba kuanzia sasa tunapoanza utekelezaji wa Sheria hii, yeyote atakayebainika kuendeleza vitendo viovu kwa watoto atakuwa amegusa mboni ya jicho la Serikali.
“Adhabu kali itatolewa kwa yeyote atakayehusika na ukatili wa aina yoyote dhidi ya watoto. Kwa wale waliojenga mazoea ya kuwaonea watoto sasa waache mara moja, kwa sababu Sheria hii sasa itachukua mkondo wake," alisema.
Sheria ya Mtoto ya mwaka 2009, inayozingatia upatikanaji wa haki za msingi za watoto na kuendeleza ustawi wao, inachukua nafasi ya Sheria tano ambazo zilifutwa na nyingine tano zilizofanyiwa marekebisho. Inaweka kuwa mtoto ni yule mwenye umri wa miaka 18 na kurudi chini.
Ilipitishwa na Bunge katika mkutano wa 17 Novemba mwaka jana na kuanza kufanyakazi rasmi Aprili 1, mwaka huu baada ya kutiwa saini na Mhe. Rais.
Kumekuwa na lawama nchini kuwa watoto wamekuwa wakinyimwa haki zao za msingi zikiwemo za kuishi, kupata elimu, kuendelezwa na kulindwa na kutunzwa.
Maandamano hayo yaliwashirikisha zaidi ya watoto 27,000 wa shule za Msingi na Sekondari wa Dodoma, kuwawakilisha watoto wenzao nchini kote.