Wednesday, May 05, 2010

 
SERIKALI KUSAIDIA UJENZI WA HOSPITALI YA RUFANI SINGIDA - PINDA

Sigida, may 1, 2010

WAZIRI MKUU Mizengo Pinda amesema Serikali itatafuta njia za kusaidia ujenzi wa hospitali ya Rufaa ya Singida ili iweze kukamilika haraka badala ya kusubiri sh. bilioni mbili za bajeti ya mkoa zinazotolewa na Serikali kuu kila mwaka.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa hospitali hiyo itakayogharimu sh. bilioni 80 kutakuwa na manufaa zaidi kwani kutaifanya iweze kuhudumia kanda ya kati ambayo haijawahi kuwa na hospitali ya rufaa tangu nchi ipate uhuru.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Ijumaa, Aprili 30, 2010) wakati akihutubia wakazi wa mji wa Singida katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye uwanja wa michezo wa Namfua, mjini Singida.

“Ukienda Tabora hakuna hospitali ya rufaa, Dodoma na Shinyanga nako hakuna. Manyara ndiyo kwanza wameanza kujenga hospitali yao ya mkoa… kwa hiyo hii hospitali yenu ni tegemeo la kanda ya kati yote,” alisema.

Waziri Mkuu ambaye alikuwa katika siku ya nne ya ziara yake ya siku tano mkoani hapa, alisema uzuri wa hospitali hiyo unasababishwa ukweli kwamba vifaa vya kutoa huduma vimekwishawasili ikiwa ni msaada kutoka Marekani.

Alisema hospitali ya sasa ilijengwa mwaka 1954 wakati huo mkoa wa Singida ukiwa na wakazi 300,000 tu lakini sasa ni zaidi ya milioni moja. Kwa hiyo imelazimu miundombinu iongezeke na hospitali hiyo ya rufaa itaiokoa hiyo ya mkoa.

Mapema jana mchana, Waziri Mkuu alitembelea hospitali hiyo iliyoko kata ya Mandewa katika Manispaa ya Singida na kuweka jiwe la msingi katika majengo ya wagonjwa wa nje na wodi ya wazazi.

Alisifu juhudi za mkoa huo kwa kuwa na idadi ndogo ya vifo vya wanawake wajawazito ambapo mkoa huo takwimu zaker zinaonyesha kuwa mwaka 2005 kulikuwa na vifo 233 kwa kila akinamama 100,000 waliokuwa wanajifungua ikilinganishwa na takwimu za kitaifa mabzo zilikuwa ni vifo 578 kwa akila akinamama 100,000 waliokuwa wanajifungua.

“Hivi sasa idadi imeshuka kutoka 233 na kufikia 119 ... hii ni kwa takwimu za mwaka jana 2009, hili limenifariji sana kwani inadhihirisha kuwa akinamama wa Singida wanakwenda kujifungulia kwenye zahanati na vituo vya afya. Mmenipa faraja kuwa hili tatizo linaweza kuisha kabisa hapa nchini, kama tukidhamiria kuliondoa,” alisema.

Alisema takwimu zimeshuka pia katika idadi ya vifo vya watoto walio chini ya umri wa miaka mitano na kwamba mkoa umefanya vizuri katika usambazaji wa vyandarua ili kukabiliana na tatizo la malaria.

Leo asubuhi (Jumamosi, Mei Mosi 2010), Waziri Mkuu atafanya majumuisho ya ziara yake katika mkoa huo kwenye ukumbi wa mikutano wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi (FDC) Singida na kisha kuelekea Dodoma akiwa njiani kurejea jijini Dar es Salaam.

Comments: Post a Comment



<< Home

This page is powered by Blogger. Isn't yours?